Waroma 12:3-13
Waroma 12:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha. Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema. Pendaneni kindugu; kila mmoja amfikirie kwanza mwenzake kwa heshima. Msilegee katika bidii, ila muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana. Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima. Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
Waroma 12:3-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinuie makuu kupita ilivyompasa kunuia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa ni unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa ni huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; msimamizi, na asimamie kwa bidii; anayerehemu, na arehemu kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkilishika lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, bila kulegea; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; mkidumu katika kusali; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.
Waroma 12:3-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.
Waroma 12:3-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha. Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.