Waroma 12:13-21
Waroma 12:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi. Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili. Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Waroma 12:13-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni. Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu. Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. Badala yake: “Kama adui yako ana njaa, mlishe; kama ana kiu, mpe kinywaji. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.” Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Waroma 12:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote. Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.” Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.” Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.
Waroma 12:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi. Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinuie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili. Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Ikiwezekana, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.