Waroma 12:1-7
Waroma 12:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msifuate kanuni za dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinuie makuu kupita ilivyompasa kunuia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa ni unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa ni huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake
Waroma 12:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake
Waroma 12:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu. Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe
Waroma 12:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja. Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.