Waroma 10:8-18
Waroma 10:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.” Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini wote hawakuipokea hiyo habari njema. Maana Isaya alisema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu.”
Waroma 10:8-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini yanenaje? Lile neno liko karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, hutokana na kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani kote, Na maneno yao hadi katika miisho ya ulimwengu.
Waroma 10:8-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Waroma 10:8-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.” Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!” Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.”