Waroma 10:5-13
Waroma 10:5-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo. Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, kumleta Kristo chini), au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.) Lakini yanenaje? Lile neno liko karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
Waroma 10:5-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini) “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.) Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, lile neno la imani tunalolihubiri. Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”
Waroma 10:5-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Kuhusu kuwa mwadilifu kwa kuitii sheria, Mose aliandika hivi: “Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya sheria ataishi.” Lakini kuhusu kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: “Usiseme moyoni mwako: ‘Nani atapanda mpaka mbinguni?’ (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: ‘Nani atashuka mpaka kuzimu?’ (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu).” Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.”
Waroma 10:5-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo. Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.) Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.