Waroma 10:17-21
Waroma 10:17-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu.” Tena nauliza: Je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni wa kwanza kujibu: “Nitawafanyeni muwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu.” Tena Isaya anathubutu hata kusema: “Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionesha kwao wasiouliza habari zangu.” Lakini kuhusu Israeli anasema: “Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii.”
Waroma 10:17-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi imani, hutokana na kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani kote, Na maneno yao hadi katika miisho ya ulimwengu. Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawakasirisha. Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nilipatikana nao wasionitafuta, Nilidhihirika kwao wasioniulizia. Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.
Waroma 10:17-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha. Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia. Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.
Waroma 10:17-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.” Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale ambao si taifa. Nitawakasirisha kwa taifa lile lisilo na ufahamu.” Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakunitafuta.” Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyooshea watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”