Waroma 10:11-17
Waroma 10:11-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.” Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini wote hawakuipokea hiyo habari njema. Maana Isaya alisema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.
Waroma 10:11-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, hutokana na kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Waroma 10:11-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
Waroma 10:11-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kama yasemavyo Maandiko, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.” Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!” Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.