Ufunuo 8:6-13
Ufunuo 8:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo. Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto pamoja na damu ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua na majani yote mabichi yakaungua. Kisha malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu, theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa, na theluthi moja ya meli zikaharibiwa. Kisha, malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto ikaanguka kutoka mbinguni na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji. (Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu. Kisha, malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku. Kisha, nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani, anasema kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!”
Ufunuo 8:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajiweka tayari ili wazipige. Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyochangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea. Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu. Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya meli zikaharibiwa. Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji. Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalifanywa kuwa machungu. Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, na usiku vivyo hivyo. Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti za baragumu ziliobakia za malaika watatu, walio tayari kupiga.
Ufunuo 8:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige. Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea. Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu. Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa. Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji. Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu. Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo. Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga.
Ufunuo 8:6-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi wale malaika saba waliokuwa na zile tarumbeta saba wakajiandaa kuzipiga. Malaika wa kwanza akaipiga tarumbeta yake, pakatokea mvua ya mawe na moto uliochanganyika na damu, navyo vikatupwa kwa nguvu juu ya nchi. Na theluthi ya dunia ikateketea, theluthi ya miti ikateketea, na nyasi yote mbichi ikateketea. Malaika wa pili akaipiga tarumbeta yake na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi ya bahari ikawa damu, theluthi ya viumbe vyenye uhai viishivyo baharini vikafa na theluthi ya meli zikaharibiwa. Malaika wa tatu akaipiga tarumbeta yake, na nyota kubwa iliyokuwa ikiwaka kama taa ikaanguka toka angani, ikaangukia theluthi ya mito na chemchemi za maji. Nyota hiyo inaitwa Uchungu. Theluthi ya maji yakawa machungu na watu wengi wakafa kutokana na maji hayo kwa maana yalikuwa machungu. Kisha malaika wa nne akaipiga tarumbeta yake, na theluthi ya jua, theluthi ya mwezi na theluthi ya nyota zikapigwa. Kwa hiyo theluthi moja ya mwanga ikawa giza. Theluthi ya mchana ikawa haina mwanga na pia theluthi ya usiku. Nilipokuwa tena nikitazama, nikamsikia tai mmoja akipiga kelele kwa sauti kuu wakati akiruka katikati ya mbingu, akisema, “Ole! Ole! Ole wa watu waishio duniani, kwa sababu ya tarumbeta ambazo malaika hao wengine watatu wanakaribia kuzipiga!”