Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 5:6-13

Ufunuo 5:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwanakondoo amesimama, akizungukwa kila upande na wale viumbe hai wanne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani. Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, wale viumbe hai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu. Basi, wakaimba wimbo huu mpya: “Wewe wastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu wetu watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Umewafanya ufalme wa makuhani wamtumikie Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha enzi, wale viumbe hai wanne na wale wazee; wakasema kwa sauti kuu: “Mwanakondoo aliyechinjwa anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, utukufu na sifa.” Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini ya dunia na baharini – viumbe vyote ulimwenguni – vikisema: “Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu na enzi, milele na milele.”

Shirikisha
Soma Ufunuo 5

Ufunuo 5:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote. Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi. Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi. Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.

Shirikisha
Soma Ufunuo 5

Ufunuo 5:6-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote. Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuzivunja lakiri zake, kwa sababu ulichinjwa na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa. Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani wa kumtumikia Mungu wetu, nao watatawala duniani.” Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema: “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa, kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na sifa!” Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba: “Sifa na heshima na utukufu na uweza ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi na kwa Mwana-Kondoo, milele na milele!”

Shirikisha
Soma Ufunuo 5

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha