Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 5:1-9

Ufunuo 5:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha nikaona kitabu katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa kwa mihuri saba. Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa: “Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?” Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani. Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili kukifungua, au kukitazama ndani. Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama! Simba wa kabila la Yuda, chipukizi wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu.” Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwanakondoo amesimama, akizungukwa kila upande na wale viumbe hai wanne, na wale wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa zimepelekwa kila mahali duniani. Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi. Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, wale viumbe hai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya Mwanakondoo. Kila mmoja alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu. Basi, wakaimba wimbo huu mpya: “Wewe wastahili kukitwaa hicho kitabu na kuivunja mihuri yake. Kwa sababu wewe umechinjwa, na kwa damu yako umemnunulia Mungu wetu watu kutoka kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Shirikisha
Soma Ufunuo 5

Ufunuo 5:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na upande wa nje, kikiwa kimefungwa kwa lakiri saba. Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, akisema, “Ni nani anayestahili kuzivunja hizo lakiri na kukifungua kitabu?” Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu wala hata kutazama ndani yake. Nikalia sana sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja hizo lakiri zake saba.” Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne na miongoni mwa wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba za Mungu zilizotumwa duniani pote. Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka kwenye mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema: “Wewe unastahili kukitwaa kitabu na kuzivunja lakiri zake, kwa sababu ulichinjwa na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu kutoka kila kabila, kila lugha, kila jamaa na kila taifa.

Shirikisha
Soma Ufunuo 5