Ufunuo 4:7-11
Ufunuo 4:7-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ngʼombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.” Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema: “Bwana wetu na Mungu wetu, wewe unastahili kupokea utukufu na heshima na uweza, kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa mapenzi yako viliumbwa na vimekuwako.”
Ufunuo 4:7-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Kiumbe wa kwanza alikuwa kama simba, wa pili kama ng'ombe, wa tatu alikuwa na sura ya mtu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. Viumbe hao wanne walikuwa na mabawa sita kila mmoja, na walikuwa wamejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika, huimba: “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu, Bwana, Mungu Mwenye Nguvu, aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!” Kila mara viumbe hao wanne walipomtukuza na kumheshimu na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi ambaye anaishi milele na milele, wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema: “Wastahili ee Bwana na Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu. Maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.”
Ufunuo 4:7-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao hutupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.
Ufunuo 4:7-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.