Ufunuo 20:4-15
Ufunuo 20:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa miaka 1,000. (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka 1,000 itimie). Huu ndio ufufuo wa kwanza. Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka 1,000. Wakati miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake. Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani. Walipita katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watakatifu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza. Naye Ibilisi aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa linalowaka madini ya kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, milele na milele. Kisha, nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena. Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uhai, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo. Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; Kifo na Kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake. Kisha Kifo na Kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili. Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uhai, alitupwa katika ziwa la moto.
Ufunuo 20:4-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha nikaona viti vya enzi vilivyokuwa vimekaliwa na hao waliopewa mamlaka ya kuhukumu, na nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudu huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye vipaji vya nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Kristo miaka 1,000. (Wafu waliosalia hawakufufuka mpaka ilipotimia hiyo miaka 1,000.) Huu ndio ufufuo wa kwanza. Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka 1,000. Hiyo miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake, naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani, Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko pwani. Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza. Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo usiku na mchana, milele na milele. Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.
Ufunuo 20:4-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa mamlaka ya kutoa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala kuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliobakia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari. Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele. Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, kulingana na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.
Ufunuo 20:4-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari. Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele. Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.