Ufunuo 2:1-5
Ufunuo 2:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika: “Mimi nishikaye zile nyota saba katika mkono wangu wa kulia na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu, nasema hivi: Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo. Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo. Lakini ninalo jambo moja dhidi yako: Wewe hunipendi tena sasa kama pale awali. Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukatubu na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa mahali pake.
Ufunuo 2:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kulia, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Ninayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wanaojiita mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
Ufunuo 2:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
Ufunuo 2:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika: “Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka. “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.