Ufunuo 18:18-24
Ufunuo 18:18-24 Biblia Habari Njema (BHN)
na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti: “Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!” Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na kuomboleza: “Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa saa moja tu umepoteza kila kitu! “Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo uliyowatenda nyinyi!” Kisha, malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe mfano wa jiwe kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, “Ndivyo Babuloni atakavyotupwa na kupotea kabisa. Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikika tena ndani yako. Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!” Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu ya watakatifu na ya watu wote waliouawa duniani.
Ufunuo 18:18-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio kama mji huu mkubwa! Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa. Furahini juu yake, enyi mbingu, na enyi watakatifu, mitume na manabii; kwa maana Mungu ametoa hukumu kwa ajili yenu juu yake. Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa. Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikika ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yoyote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana arusi na bibi arusi haitasikika ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako. Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.
Ufunuo 18:18-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
wakalia sana, walipouona moshi wa kuungua kwake, wakisema, Ni mji upi ulio mfano wa mji huu mkubwa! Wakatupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wakalia, wakitokwa na machozi na kuomboleza, wakisema, Ole, ole, mji ule ulio mkuu! Ambao ndani yake wote wenye merikebu baharini walipata mali kwa utajiri wake; kwa kuwa katika saa moja umekuwa ukiwa. Furahini juu yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na manabii; kwa maana Mungu amehukumu hukumu yenu juu yake. Na malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe, kama jiwe kubwa la kusagia, akalitupa katika bahari, akisema, Kama hivi, kwa nguvu nyingi, utatupwa Babeli, mji ule mkuu, wala hautaonekana tena kabisa. Wala sauti ya wapiga vinanda, na ya wapiga zomari, na ya wapiga filimbi, na ya wapiga baragumu, haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala fundi awaye yote wa kazi yo yote hataonekana ndani yako tena kabisa; wala sauti ya jiwe la kusagia haitasikiwa ndani yako tena kabisa; wala nuru ya taa haitamulika ndani yako tena kabisa; wala sauti ya bwana-arusi na bibi-arusi haitasikiwa ndani yako tena kabisa; maana hao wafanya biashara wako walikuwa wakuu wa nchi, kwa kuwa mataifa yote walidanganywa kwa uchawi wako. Na ndani yake ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.
Ufunuo 18:18-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Watakapouona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’ Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema: “ ‘Ole! Ole, ee mji mkubwa, mji ambao wote wenye meli baharini walitajirika kupitia kwa mali zake! Katika saa moja tu ameangamizwa! Furahia kwa ajili yake, ee mbingu! Furahini watakatifu, mitume na manabii! Mungu amemhukumu kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ” Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema: “Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli utakavyotupwa chini kwa nguvu wala hautaonekana tena. Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji, wapiga filimbi na wapiga tarumbeta kamwe hazitasikika tena ndani yako. Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi mwenye ujuzi wa aina yoyote. Wala sauti ya jiwe la kusagia kamwe haitasikika tena. Mwanga wa taa hautaangaza ndani yako tena. Sauti ya bwana arusi na bibi arusi kamwe haitasikika ndani yako tena. Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia. Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako. Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu na wote waliouawa duniani.”