Ufunuo 12:7-12
Ufunuo 12:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake. Lakini joka hilo na malaika wake walishindwa, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yao. Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani ambaye huudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa umefika ukombozi na nguvu na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake! Maana yule aliyewashtaki ndugu zetu mbele ya Mungu ametupwa chini. Naam, ametupwa chini huyo anayewashtaki usiku na mchana. Ndugu zetu wamemshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno waliloshuhudia; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa. Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba muda wake uliobakia ni mfupi.”
Ufunuo 12:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika wake wakapigana na lile joka, lile joka nalo likapigana nao pamoja na malaika wake; lakini hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Lile joka kuu likatupwa, yule nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika wake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu akiwa na ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.
Ufunuo 12:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.
Ufunuo 12:7-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake. Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema: “Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja na mamlaka ya Kristo wake. Kwa kuwa ametupwa chini mshtaki wa ndugu zetu, anayewashtaki mbele za Mungu usiku na mchana. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo na kwa neno la ushuhuda wao. Wala wao hawakuyapenda maisha yao hata kufa. Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu na wote wakaao humo! Lakini ole wenu nchi na bahari, kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu, akiwa amejaa ghadhabu, kwa sababu anajua ya kuwa muda wake ni mfupi!”