Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 9:1-20

Zaburi 9:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu. Wakati ulipotokea, maadui zangu walirudi nyuma, walijikwaa na kuangamia. Umenitetea kuhusu kisa changu cha haki; umeketi katika kiti chako cha enzi, ukatoa hukumu iliyo sawa. Umeyakemea mataifa, umewaangamiza waovu; majina yao umeyafutilia mbali milele. Maadui wameangamia milele; umeingolea mbali miji yao, kumbukumbu lao limetoweka. Lakini Mwenyezi-Mungu anatawala milele; ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu. Anauhukumu ulimwengu kwa haki; anayaamua mataifa kwa unyofu. Mwenyezi-Mungu ni ngome ya watu wanaoonewa; yeye ni ngome nyakati za taabu. Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea, wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao. Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni. Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda! Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu; kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa. Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu! Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia; wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo, nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni, nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa. Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba, wamenaswa miguu katika wavu waliouficha. Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo; ametekeleza hukumu. Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe. Waovu wataishia kuzimu; naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu. Lakini fukara hawatasahauliwa daima; tumaini la maskini halitapotea milele. Inuka, ee Mwenyezi-Mungu! Usimwache binadamu ashinde. Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu. Uyatie hofu, ee Mwenyezi-Mungu, watu wa mataifa watambue kuwa wao ni watu tu!

Shirikisha
Soma Zaburi 9

Zaburi 9:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu; Nitafurahi na kukushangilia; Nitaliimbia sifa jina lako, Wewe Uliye juu. Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako. Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki. Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele; Adui wameangamia na kuwa magofu milele. Nayo miji yao uliing'oa; Hata kumbukumbu lao limepotea. Bali BWANA atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu. Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa uadilifu. BWANA atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida. Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, BWANA hukuwaacha wakutafutao. Mwimbieni BWANA akaaye Sayuni, Yatangazeni kwa watu matendo yake. Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge. Wewe, BWANA, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti, Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako. Mataifa wamezama katika shimo walilolichimba; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao. BWANA amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake. Wadhalimu wataenda kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. Inuka, ee BWANA, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako. Uwatie hofu, ee BWANA, Watu wa mataifa na wajitambue kuwa wao ni binadamu tu!

Shirikisha
Soma Zaburi 9

Zaburi 9:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote; Nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu; Nitafurahi na kukushangilia Wewe; Nitaliimbia jina lako, Wewe Uliye juu. Kwa sababu adui zangu hurudi nyuma; Hujikwaa na kuangamia mbele zako. Kwa maana umenifanyia hukumu na haki Umeketi kitini pa enzi ukihukumu kwa haki. Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele; Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele. Nayo miji yao uliing’oa; Hata kumbukumbu lao limepotea. Bali BWANA atakaa milele, Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu. Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili. BWANA atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida. Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, BWANA hukuwaacha wakutafutao. Mwimbieni BWANA akaaye Sayuni, Yatangazeni kati ya watu matendo yake. Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge. Wewe, BWANA, unifadhili, Tazama mateso niteswayo na wanaonichukia; Wewe uniinuaye katika malango ya mauti, Ili nizisimulie sifa zako zote; Katika malango ya binti Sayuni Nitaufurahia wokovu wako. Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao. BWANA amejidhihirisha na kutekeleza hukumu; Amemnasa mdhalimu kwa kazi ya mikono yake. Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. Kwa maana mhitaji hatasahauliwa daima; Matumaini ya wanyonge hayatapotea milele. BWANA, usimame, mwanadamu asipate nguvu, Mataifa wahukumiwe mbele zako. BWANA, uwawekee kitisho, Mataifa na wajijue kuwa ni binadamu.

Shirikisha
Soma Zaburi 9

Zaburi 9:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee BWANA, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana. Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako. Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki. Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele. Uharibifu usiokoma umempata adui, umeingʼoa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka. BWANA anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu. Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki. BWANA ni kimbilio la watu wanaoonewa, ni ngome imara wakati wa shida. Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe BWANA, hujawaacha kamwe wakutafutao. Mwimbieni BWANA sifa, amefanywa mtawala Sayuni, tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda. Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka, hapuuzi kilio cha wanaoonewa. Ee BWANA, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa! Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti, ili niweze kutangaza sifa zako katika malango ya Binti Sayuni na huko niushangilie wokovu wako. Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha. BWANA anajulikana kwa haki yake, waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao. Waovu wataishia kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea. Ee BWANA, inuka, usimwache binadamu ashinde. Mataifa na yahukumiwe mbele zako. Ee BWANA, wapige kwa hofu, mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu.

Shirikisha
Soma Zaburi 9

Zaburi 9:1-20

Zaburi 9:1-20 BHNZaburi 9:1-20 BHNZaburi 9:1-20 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha