Zaburi 78:9-16
Zaburi 78:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kufuata sheria yake; Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonesha. Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. Aliipasua bahari akawavusha; Aliyafanya maji yasimame kama ukuta. Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. Akafanya vijito vitokeze katika mwamba, Na kufanya maji yatiririke kama mito.
Zaburi 78:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu wa Efraimu, pinde na mishale mkononi, walirudi nyuma, wakakimbia siku ile ya vita. Hawakulizingatia agano la Mungu; walikataa kufuata sheria yake. Walisahau mambo aliyokuwa ametenda, miujiza aliyokuwa amewaonesha. Alifanya maajabu mbele ya wazee wao, kondeni Soani, nchini Misri. Aliigawa bahari, akawapitisha humo; aliyafanya maji yasimame kama ukuta. Mchana aliwaongoza kwa wingu; usiku kucha kwa mwanga wa moto. Aliipasua miamba kule jangwani, akawanywesha maji kutoka vilindini. Alibubujisha vijito kutoka mwambani, akatiririsha maji kama mito.
Zaburi 78:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wale Waefraimu, wenye silaha, wapiga upinde, Walirudi nyuma siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu; Wakakataa kuenenda katika sheria yake; Wakayasahau matendo yake, Na mambo yake ya ajabu aliyowaonyesha. Mbele ya baba zao alifanya mambo ya ajabu, Katika nchi ya Misri, konde la Soani. Aliipasua bahari akawavusha; Aliyasimamisha maji mfano wa chungu. Akawaongoza kwa wingu mchana, Na usiku kucha kwa nuru ya moto. Akapasua miamba jangwani; Akawanywesha maji mengi kama maji ya vilindi. Akatokeza na vijito gengeni, Akatelemsha maji kama mito.
Zaburi 78:9-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde, walikimbia siku ya vita. Hawakulishika agano la Mungu na walikataa kuishi kwa sheria yake. Walisahau aliyokuwa ameyatenda, maajabu aliyokuwa amewaonyesha. Alitenda miujiza machoni mwa baba zao, huko Soani, katika nchi ya Misri. Aliigawanya bahari akawapitisha, alifanya maji yasimame imara kama ukuta. Aliwaongoza kwa wingu mchana na kwa nuru kutoka kwenye moto usiku kucha. Alipasua miamba jangwani na akawapa maji tele kama bahari, alitoa vijito kutoka kwenye jabali lililochongoka, akayafanya maji yatiririke kama mito.