Zaburi 62:1-5
Zaburi 62:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa utulivu, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika. Hadi lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama ua ulio tayari kuanguka, Mpango wao ni kumwangusha tu mtu mwenye cheo; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani. Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa utulivu. Maana tumaini langu hutoka kwake.
Zaburi 62:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu, kwake watoka wokovu wangu. Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu, yeye ni ngome yangu, sitatikisika. Hata lini mtanishambulia mimi? Hata lini nyinyi nyote mtanipiga, mimi niliye kama kiambaza kilichoinama, kama ukuta unaoanza kubomoka? Mmepanga kuniangusha toka mahali pangu pa heshima; furaha yenu ni kusema uongo. Kwa maneno, mnabariki, lakini moyoni mnalaani. Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu; kwake naliweka tumaini langu.
Zaburi 62:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. Hata lini mtamshambulia mtu, Mpate kumwua ninyi nyote pamoja? Kama ukuta unaoinama, Kama kitalu kilicho tayari kuanguka, Hufanya shauri kumwangusha tu katika cheo chake; Huufurahia uongo. Kwa kinywa chao hubariki; Kwa moyo wao hulaani. Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake.
Zaburi 62:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko; wokovu wangu watoka kwake. Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe. Mtamshambulia mtu hata lini? Je, ninyi nyote mtamtupa chini, ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika? Walikusudia kikamilifu kumwangusha toka mahali pake pa fahari; wanafurahia uongo. Kwa vinywa vyao hubariki, lakini ndani ya mioyo yao hulaani. Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake, tumaini langu latoka kwake.