Zaburi 48:1-14
Zaburi 48:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu, ni mkuu; astahili kusifiwa sana katika mji wake na mlima wake mtakatifu. Mlima Siyoni huko kaskazini, wapendeza kwa urefu; mji wa Mfalme mkuu ni furaha ya ulimwengu. Mungu anazilinda ngome zake; yeye amejionesha kuwa ngome ya usalama. Wafalme walikusanyika, wakaenda pamoja kushambulia. Lakini walipouona mji wa Siyoni, wakashangaa; wakashikwa na hofu, wakatimua mbio. Hofu kuu iliwashika, wakasikia uchungu kama mama anayejifungua, kama waliokumbwa na kimbunga cha mashariki ambacho huzivunjavunja meli za Tarshishi. Yote tuliyosikia tumejionea wenyewe katika mji wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, naam, katika mji wa Mungu wetu; Mungu atauimarisha milele. Ee Mungu, twazitafakari fadhili zako, tukiwa hekaluni mwako. Jina lako lasifika kila mahali, sifa zako zaenea popote duniani. Kwa mkono wako umetenda kwa haki; watu wa Siyoni na wafurahi! Watu wa Yuda na washangilie, kwa sababu ya maamuzi yako ya haki! Tembeeni huko Siyoni mkauzunguke, mkaihesabu minara yake. Zitazameni kuta zake na kuchunguza ngome zake; mpate kuvisimulia vizazi vijavyo, kwamba: “Huyu ni Mungu, Mungu wetu milele! Atakuwa kiongozi wetu milele!”
Zaburi 48:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana ndiye aliye mkuu, Na mwenye kusifiwa sana. Katika mji wa Mungu wetu, Katika mlima wake mtakatifu. Kuinuka kwake ni mzuri sana, Ni furaha ya dunia yote. Mlima Sayuni, kule upande wa kaskazini, Mji wa Mfalme mkuu. Mungu katika majumba yake Amejijulisha kuwa ngome. Maana, tazama, wafalme walikusanyika; Walikuja wote pamoja. Mara Walipouona, wakashtuka; Wakafadhaika na kukimbia. Papo hapo tetemeko liliwashika, Uchungu kama wa mwanamke azaaye. Kama upepo wa mashariki Unapovunja jahazi za Tarshishi. Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona, Katika mji wa BWANA wa majeshi. Mji wa Mungu wetu; Mungu atauimarisha hata milele. Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu, Katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu, Ndivyo na sifa yako hadi miisho ya dunia. Mkono wako wa kulia umejaa haki; Na ufurahi mlima Sayuni. Binti za Yuda na washangilie Kwa sababu ya hukumu zako. Tembeeni katika Sayuni, Uzungukeni mji wote, Ihesabuni minara yake, Tieni moyoni boma zake, Yafikirini majumba yake, Mpate kuwaambia kizazi kitakachokuja. Kwa maana ndivyo alivyo MUNGU, Mungu wetu. Milele na milele Yeye ndiye atakayetuongoza.
Zaburi 48:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana ndiye aliye mkuu, Na mwenye kusifiwa sana. Katika mji wa Mungu wetu, Katika mlima wake mtakatifu. Kuinuka kwake ni mzuri sana, Ni furaha ya dunia yote. Mlima Sayuni pande za kaskazini, Mji wa Mfalme mkuu. Mungu katika majumba yake Amejijulisha kuwa ngome. Maana, tazama, wafalme walikusanyika; Walipita wote pamoja. Waliona, mara wakashangaa; Wakafadhaika na kukimbia. Papo hapo tetemeko liliwashika, Utungu kama wa mwanamke azaaye. Kwa upepo wa mashariki Wavunja jahazi za Tarshishi. Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona, Katika mji wa BWANA wa majeshi. Mji wa Mungu wetu; Mungu ataufanya imara hata milele. Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu, Katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu, Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki; Na ufurahi mlima Sayuni. Binti za Yuda na washangilie Kwa sababu ya hukumu zako. Tembeeni katika Sayuni, Uzungukeni mji, Ihesabuni minara yake, Tieni moyoni boma zake, Yafikirini majumba yake, Mpate kuwaambia kizazi kitakachokuja. Kwa maana ndivyo alivyo MUNGU, Mungu wetu. Milele na milele Yeye ndiye atakayetuongoza.
Zaburi 48:1-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu, mlima wake mtakatifu. Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana, furaha ya dunia yote. Kama vilele vya juu sana vya Safoni ni Mlima Sayuni, mji wa Mfalme Mkuu. Mungu yuko katika ngome zake; amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake. Wakati wafalme walipounganisha nguvu, waliposonga mbele pamoja, walimwona nao wakashangaa, wakakimbia kwa hofu. Kutetemeka kuliwashika huko, maumivu kama ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa. Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi zilizovunjwa na upepo wa mashariki. Kama tulivyokuwa tumesikia, ndivyo tulivyoona katika mji wa BWANA Mwenye Nguvu Zote, katika mji wa Mungu wetu: Mungu ataufanya uwe salama milele. Ee Mungu, hekaluni mwako tunatafakari upendo wako usiokoma. Ee Mungu, kama jina lako lilivyo, sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia, mkono wako wa kuume umejazwa na haki. Mlima Sayuni unashangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako. Tembeeni katika Sayuni, uzungukeni mji, hesabuni minara yake; yatafakarini vyema maboma yake, angalieni ngome zake, ili mpate kusimulia habari zake kwa kizazi kijacho. Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.