Zaburi 22:1-11
Zaburi 22:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mbona uko mbali sana kunisaidia, mbali na maneno ya kilio changu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu; napiga yowe usiku, lakini nafuu sipati. Hata hivyo, wewe ni mtakatifu; wewe watawala na kusifiwa na Waisraeli. Wazee wetu walikutegemea; walikutegemea, nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe, wakaokolewa; walikutegemea, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu tu, wala si mtu; nimepuuzwa na kudharauliwa na watu. Wote wanionao hunidhihaki; hunifyonya na kutikisa vichwa vyao. Husema: “Alimtegemea Mwenyezi-Mungu, basi, Mungu na amkomboe! Kama Mungu anapendezwa naye, basi, na amwokoe!” Lakini ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, uliniweka salama kifuani pa mama yangu. Nimekutegemea tangu kuzaliwa kwangu. Tangu nilipozaliwa wewe umekuwa Mungu wangu. Usikae mbali nami, kwani taabu imekaribia; wala hakuna wa kunisaidia.
Zaburi 22:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Lakini Wewe U Mtakatifu, Utukuzwaye na sifa za Israeli. Baba zetu walikutumainia Wewe, Walitumainia, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumainia, nao hawakuaibika. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Nimedharauliwa na kupuuzwa na watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee BWANA; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinisalimisha matitini mwa mama yangu. Kwako nilitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.
Zaburi 22:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema, Umtegemee BWANA; na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Naam, Wewe ndiwe uliyenitoa tumboni, Ulinitumainisha matitini mwa mama yangu. Kwako nalitupwa tangu tumboni, Toka tumboni mwa mamangu ndiwe Mungu wangu. Usiwe mbali nami maana taabu i karibu, Kwa maana hakuna msaidizi.
Zaburi 22:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi. Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli. Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa. Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika. Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau. Wote wanionao hunidhihaki, hunivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao: Husema, “Anamtegemea BWANA, basi BWANA na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.” Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu. Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu. Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia.