Zaburi 18:43-50
Zaburi 18:43-50 Biblia Habari Njema (BHN)
Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu, ukanifanya mtawala wa mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Mara waliposikia habari zangu walinitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni walikufa moyo; wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka. Mwenyezi-Mungu yu hai! Asifiwe mwamba wa usalama wangu; atukuzwe Mungu wa wokovu wangu. Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi; na kuyashinda mataifa chini yangu. Ameniokoa kutoka kwa maadui zangu, akanikuza juu ya wapinzani wangu, na kunisalimisha mbali na watu wakatili. Kwa hiyo nitakutukuza kati ya mataifa, ee Mwenyezi-Mungu nitaliimbia sifa jina lako. Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa; humwonesha fadhili zake huyo mteule wake, naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.
Zaburi 18:43-50 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Umeniokoa kutoka kwa mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Mara tu waliposikia habari zangu, wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; Ndiye Mungu anilipizaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu mjeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na wazawa wake hata milele.
Zaburi 18:43-50 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri. Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake, Daudi na mzao wake hata milele.
Zaburi 18:43-50 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa, watu ambao sikuwajua wananitumikia. Mara wanisikiapo hunitii, wageni hunyenyekea mbele yangu. Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu! Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, awatiishaye mataifa chini yangu, aniokoaye na adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee BWANA; nitaliimbia sifa jina lako. Humpa mfalme wake ushindi mkuu, huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele.