Zaburi 16:1-11
Zaburi 16:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Unilinde ee Mungu; maana kwako nakimbilia usalama. Namwambia Mungu: “Wewe u Bwana wangu; sina jema lolote ila wewe.” Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini, kukaa nao ndiyo furaha yangu. Lakini wanaoabudu miungu mingine, watapata mateso mengi. Tambiko ya damu sitaitolea kamwe, na majina ya miungu hiyo sitayataja. Wewe ee Mwenyezi-Mungu ndiwe riziki yangu kuu, majaliwa yangu yamo mikononi mwako. Umenipimia sehemu nzuri sana; naam, urithi wangu ni wa kupendeza. Namsifu Mwenyezi-Mungu kwa kuniongoza, usiku dhamiri yangu yanionya. Namweka Mwenyezi-Mungu mbele yangu daima; yuko pamoja nami, wala sitatikisika. Kwa hiyo nitafurahi kwa moyo wote na kushangilia, nami nitakaa salama salimini. Naam wewe hutaiacha nafsi yangu kuzimu, hutaniacha mimi mwaminifu wako nipate kuoza. Wanionesha njia ya kufikia uhai; kuwako kwako kwanijaza furaha kamili, katika mkono wako wa nguvu mna mema ya milele.
Zaburi 16:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu; Sina wema ila utokao kwako. Nao watakatifu waliopo duniani, ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao. Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu. BWANA ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unayaamua maisha yangu. Mipaka yangu imeangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri. Nitamhimidi BWANA aniongozaye, Wakati wa usiku pia moyo wangu hunishauri. Nimemweka BWANA mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuliani mwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nayo nafsi yangu inashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini. Maana hutaitupa kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako kuna furaha tele; Na katika mkono wako wa kulia Mna mema ya milele.
Zaburi 16:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu; Sina wema ila utokao kwako. Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao. Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu. BWANA ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu. Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri. Nitamhimidi BWANA aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. Nimemweka BWANA mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini. Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
Zaburi 16:1-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia. Nilimwambia BWANA, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.” Kwa habari ya watakatifu walioko duniani, ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao. Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka zao za damu au kutaja majina yao midomoni mwangu. BWANA umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama. Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri. Nitamsifu BWANA ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha. Nimemweka BWANA mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama, kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu. Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha za milele katika mkono wako wa kuume.