Zaburi 147:2-11
Zaburi 147:2-11 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
BWANA hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni. Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao. Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake. Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo. BWANA huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini. Mwimbieni BWANA kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi. Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima. Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia. Furaha yake haipo katika nguvu za farasi, wala furaha yake kwenye miguu ya mwanadamu. BWANA hupendezwa na wale wamchao, wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.
Zaburi 147:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake.
Zaburi 147:2-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuyaganga majeraha yao. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka. BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. Mwimbieni BWANA kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuichipusha nyasi milimani. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao. Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mkimbiaji. BWANA huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.
Zaburi 147:2-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka. BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. Mwimbieni BWANA kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao. Hapendezwi na nguvu za farasi, Wala hairidhii miguu ya mtu. BWANA huwaridhia wao wamchao, Na kuzitarajia fadhili zake.