Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 147:1-20

Zaburi 147:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia. Yeye hataki nguvu za farasi, wala hapendezwi na ushujaa wa askari; lakini hupendezwa na watu wamchao, watu wanaotegemea fadhili zake. Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu! Umsifu Mungu wako, ee Siyoni! Maana yeye huimarisha milango yako, huwabariki watu waliomo ndani yako. Huweka amani mipakani mwako; hukushibisha kwa ngano safi kabisa. Yeye hupeleka amri yake duniani, na neno lake hufikia lengo lake haraka. Hutandaza theluji kama pamba, hutawanya umande kama majivu. Huleta mvua ya mawe kama kokoto na kwa ubaridi wake maji huganda. Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka; huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka. Humjulisha Yakobo ujumbe wake, na Israeli masharti na maagizo yake. Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine; watu wengine hawayajui maagizo yake. Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Shirikisha
Soma Zaburi 147

Zaburi 147:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Msifuni BWANA. Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa, jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye! BWANA hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni. Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao. Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake. Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo. BWANA huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini. Mwimbieni BWANA kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi. Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima. Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia. Furaha yake haipo katika nguvu za farasi, wala furaha yake kwenye miguu ya mwanadamu. BWANA hupendezwa na wale wamchao, wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma. Mtukuze BWANA, ee Yerusalemu, msifu Mungu wako, ee Sayuni, kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako na huwabariki watu wako walio ndani yako. Huwapa amani mipakani mwenu na kukushibisha kwa ngano safi kabisa. Hutuma amri yake duniani, neno lake hukimbia kasi. Anatandaza theluji kama sufu na kutawanya umande kama majivu. Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe. Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake? Hutuma neno lake na kuviyeyusha, huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka. Amemfunulia Yakobo neno lake, sheria zake na maagizo yake kwa Israeli. Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote, hawazijui sheria zake.

Shirikisha
Soma Zaburi 147