Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 145:1-21

Zaburi 145:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu; nitalitukuza jina lako daima na milele. Nitakutukuza kila siku; nitalisifu jina lako daima na milele. Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi; ukuu wake hauwezi kuchunguzika. Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa, watu watatangaza matendo yako makuu. Nitanena juu ya utukufu na fahari yako, nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu, nami nitatangaza ukuu wako. Watatangaza sifa za wema wako mwingi, na kuimba juu ya uadilifu wako. Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema; hakasiriki ovyo, amejaa fadhili. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote, ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza. Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa. Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu, nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake. Waufumbua mkono wako kwa ukarimu, watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote; ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa. Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda; lakini atawaangamiza waovu wote. Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu; viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu, milele na milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 145

Zaburi 145:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele. BWANA ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hauchunguziki. Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu. Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu. Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako. Watasimulia juu ya ukuu wa wema wako mwingi. Na wataiimba haki yako kwa sauti. BWANA ni mwenye fadhili na huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, BWANA ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake ziko juu ya vyote alivyoumba. Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kusena uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa milele, BWANA ni mwaminifu katika maneno yake yote, Na mwenye fadhili katika matendo yake yote Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini. Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye huruma katika matendo yake yote. BWANA yuko karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. Hutimiza matakwa ya wote wamchao, Na pia husikia kilio chao, na huwaokoa. BWANA huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza. Kinywa changu kitazinena sifa za BWANA; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 145

Zaburi 145:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele. BWANA ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani. Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu. Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu. Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako. Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako. BWANA ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, BWANA ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini. Macho ya watu wote yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. BWANA yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu. Atawafanyia wamchao matakwa yao, Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa. BWANA huwahifadhi wote wampendao, Na wote wasio haki atawaangamiza. Kinywa changu kitazinena sifa za BWANA; Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 145

Zaburi 145:1-21 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme, nitalisifu jina lako milele na milele. Kila siku nitakusifu na kulitukuza jina lako milele na milele. BWANA ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, ukuu wake haupimiki. Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine, watasimulia matendo yako makuu. Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako, nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu. Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha, nami nitatangaza matendo yako makuu. Wataadhimisha wema wako mwingi, na wataimba kwa shangwe juu ya haki yako. BWANA ni mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo. BWANA ni mwema kwa wote, ana huruma kwa vyote alivyovifanya. Ee BWANA, vyote ulivyovifanya vitakusifu, watakatifu wako watakutukuza. Watasimulia utukufu wa ufalme wako na kusema juu ya ukuu wako, ili watu wote wajue matendo yako makuu na utukufu wa fahari ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele, mamlaka yako hudumu vizazi vyote. BWANA ni mwaminifu kwa ahadi zake zote na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya. BWANA huwategemeza wote waangukao, na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao. Macho yao wote yanakutazama wewe, nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai. BWANA ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya. BWANA yu karibu na wote wamwitao, karibu na wote wamwitao kwa uaminifu. Huwatimizia wamchao matakwa yao, husikia kilio chao na kuwaokoa. BWANA huwalinda wote wampendao, bali waovu wote atawaangamiza. Kinywa changu kitazinena sifa za BWANA. Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu milele na milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 145

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha