Zaburi 143:1-12
Zaburi 143:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Usikie sala yangu, ee Mwenyezi-Mungu! Ulitegee sikio ombi langu maana wewe ni mwaminifu; unijibu kwa sababu ya uadilifu wako. Usinitie hukumuni mimi mtumishi wako, maana hakuna yeyote aliye mwadilifu mbele yako. Maadui zangu wamenifuatia; wameniangusha chini kabisa wameniketisha gizani kama mtu aliyekufa zamani. Nimevunjika moyo kabisa; nimekufa ganzi kwa ajili ya woga. Nakumbuka siku zilizopita; natafakari juu ya yote uliyotenda, nawaza na kuwazua juu ya matendo yako. Nakunyoshea mikono yangu kuomba; nina kiu yako kama nchi kavu isiyo na maji. Ee Mwenyezi-Mungu, unijibu haraka; maana nimekata tamaa kabisa! Usijifiche mbali nami, nisije nikawa kama wale washukao kwa wafu. Asubuhi unioneshe fadhili zako, maana nimekuwekea tumaini langu. Unifundishe mwenendo wa kufuata, maana nakuelekezea ombi la moyo wangu. Uniokoe, ee Mwenyezi-Mungu, kutoka maadui zangu, maana kwako nakimbilia usalama. Unifundishe kutimiza matakwa yako, maana wewe ni Mungu wangu! Roho yako nzuri iniongoze katika njia sawa. Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu, kwa hisani yako, uniondoe katika taabu kwa sababu ya uadilifu wako. Kwa sababu ya fadhili zako uwakomeshe maadui zangu, uwaangamize wote wanaonidhulumu; maana mimi ni mtumishi wako.
Zaburi 143:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu Unijibu Kwa uaminifu wako, Unijibu kwa haki yako. Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki. Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umeshtuka. Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako. Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame. Ee BWANA, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni. Uniwezeshe kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unifundishe njia nitakayoiendea, Kwa maana ninakuinulia nafsi yangu. Ee BWANA, uniponye kutoka kwa adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche. Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze katika njia iliyo sawa, Ee BWANA, uniponye kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni; Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako.
Zaburi 143:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, uisikie sala yangu, uzisikilize dua zangu, Kwa uaminifu wako unijibu kwa haki yako. Wala usimhukumu mtumishi wako, Maana kwako hakuna aliye hai mwenye haki. Maana adui ameifuatia nafsi yangu, Ameutupa chini uzima wangu. Amenikalisha mahali penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Na roho yangu imezimia ndani yangu, Moyo wangu ndani yangu umesituka. Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako. Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame. Ee BWANA, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni Unifanye kusikia fadhili zako asubuhi, Kwa maana nimekutumaini Wewe. Unijulishe njia nitakayoiendea, Kwa maana nakuinulia nafsi yangu. Ee BWANA, uniponye na adui zangu; Nimekukimbilia Wewe, unifiche. Unifundishe kuyatenda mapenzi yako, Kwa maana ndiwe Mungu wangu; Roho yako mwema aniongoze kwenye nchi sawa, Ee BWANA, unihuishe kwa ajili ya jina lako, Kwa haki yako unitoe roho yangu taabuni; Kwa fadhili zako utawakatilia mbali adui zangu; Na kuwaangamiza wote wanitesao nafsi, Kwa maana mimi ni mtumishi wako.
Zaburi 143:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee BWANA, sikia sala yangu, sikiliza kilio changu unihurumie; katika uaminifu na haki yako njoo unisaidie. Usimhukumu mtumishi wako, kwa kuwa hakuna mtu anayeishi aliye mwenye haki mbele zako. Adui hunifuatilia, hunipondaponda chini; hunifanya niishi gizani kama wale waliokufa zamani. Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu, moyo wangu ndani yangu unakata tamaa. Nakumbuka siku za zamani; natafakari juu ya kazi zako zote, naangalia juu ya kazi ambazo mikono yako imezifanya. Nanyoosha mikono yangu kwako, nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame. Ee BWANA, unijibu haraka, roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, ama sivyo nitafanana na wale washukao shimoni. Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma, kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako. Nionyeshe njia nitakayoiendea, kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu. Ee BWANA, uniokoe na adui zangu, kwa kuwa nimejificha kwako. Nifundishe kufanya mapenzi yako, kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu, Roho wako mwema na aniongoze katika nchi tambarare. Ee BWANA, kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu, kwa haki yako nitoe katika taabu. Kwa upendo wako usiokoma, nyamazisha adui zangu; waangamize watesi wangu wote, kwa kuwa mimi ni mtumishi wako.