Zaburi 139:7-18
Zaburi 139:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko? Niende wapi ambako wewe huko? Nikipanda juu mbinguni, wewe upo; nikijilaza chini kuzimu, wewe upo. Nikiruka hadi mawio ya jua, au hata mipakani mwa bahari, hata huko upo kuniongoza; mkono wako wa kulia utanitegemeza. Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja. Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe.
Zaburi 139:7-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kulia utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa njia ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi katika pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Kitabuni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mawazo yako ni mazito sana kwangu; Ee Mungu; nayo ni makuu sana. Kama ningeyahesabu ni mengi kuliko mchanga; Niamkapo ningali pamoja nawe.
Zaburi 139:7-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.
Zaburi 139:7-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari, hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti. Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,” hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako. Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu. Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi, macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja. Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa! Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe.