Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 139:1-24

Zaburi 139:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali. Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote. Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee BWANA. Umenizunguka nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu. Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia. Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari, hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti. Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,” hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako. Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu. Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi, macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja. Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa! Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe. Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu! Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako. Ee BWANA, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako? Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu. Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu. Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 139

Zaburi 139:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza; wewe wanijua mpaka ndani. Nikiketi au nikisimama, wewe wajua; wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria. Watambua nikienda au nikipumzika; wewe wazijua shughuli zangu zote. Kabla sijasema neno lolote, wewe, ee Mwenyezi-Mungu, walijua kabisa. Uko kila upande wangu, mbele na nyuma; waniwekea mkono wako kunilinda. Maarifa yako yapita akili yangu; ni makuu mno, siwezi kuyaelewa. Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko? Niende wapi ambako wewe huko? Nikipanda juu mbinguni, wewe upo; nikijilaza chini kuzimu, wewe upo. Nikiruka hadi mawio ya jua, au hata mipakani mwa bahari, hata huko upo kuniongoza; mkono wako wa kulia utanitegemeza. Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja. Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe. Laiti, ee Mungu, ungewaua watu waovu! Laiti watu wauaji wangeondoka kwangu! Wanasema vibaya juu yako; wanasema maovu juu ya jina lako! Ee Mwenyezi-Mungu, nawachukia wanaokuchukia; nawadharau sana wale wanaokuasi! Maadui zako ni maadui zangu; ninawachukia kabisakabisa. Unichunguze, ee Mungu, unijue moyo wangu, unipime, uyajue mawazo yangu. Uangalie kama mwenendo wangu ni mbaya, uniongoze katika njia ya milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 139

Zaburi 139:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kusimama kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno katika ulimini wangu Usilolijua kabisa, BWANA. Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako. Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia. Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kulia utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa njia ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi katika pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Kitabuni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mawazo yako ni mazito sana kwangu; Ee Mungu; nayo ni makuu sana. Kama ningeyahesabu ni mengi kuliko mchanga; Niamkapo ningali pamoja nawe. Ee Mungu, laiti ungewaua waovu! Na laiti watu wa damu wangetoka kwangu; Wale wanaokusema kwa ubaya, na kutenda maovu juu ya jina lako bure. Je! BWANA nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiudhike nao watu wanaokuasi? Nawachukia kwa upepo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu. Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 139

Zaburi 139:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, BWANA. Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako. Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia. Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu. Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana, Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi; Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe. Ee Mungu, laiti ungewafisha waovu! Enyi watu wa damu, ondokeni kwangu; Kwa maana wakuasi kwa ubaya, Adui zako wakutaja jina lako bure. Je! BWANA nisiwachukie wanaokuchukia? Nisikirihike nao wakuasio? Nawachukia kwa ukomo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu. Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 139