Zaburi 124:1-8
Zaburi 124:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
“Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu Semeni nyote mlio katika Israeli: “Kama Mwenyezi-Mungu asingalikuwa upande wetu, wakati ule tuliposhambuliwa na maadui, hakika tungalimezwa tukiwa hai, wakati hasira zao zilipotuwakia. Tungalikumbwa na gharika, tungalifunikwa na mto wa maji, mkondo wa maji ungalituchukua!” Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, ambaye hakutuacha makuchani mwao. Tumeponyoka kama ndege mtegoni; mtego umeteguliwa, nasi tukaokoka. Msaada wetu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia.
Zaburi 124:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu. Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo maji yafurikayo Yangalipita juu yetu. Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyeziumba mbingu na nchi.
Zaburi 124:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Israeli na aseme sasa, Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo. Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.
Zaburi 124:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kama BWANA asingalikuwa upande wetu; Israeli na aseme sasa: kama BWANA asingalikuwa upande wetu, wakati watu walipotushambulia, wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu, wangalitumeza tungali hai, mafuriko yangalitugharikisha, maji mengi yangalitufunika, maji yaendayo kasi yangalituchukua. BWANA asifiwe, yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao. Tumeponyoka kama ndege kutoka mtego wa mwindaji; mtego umevunjika, nasi tukaokoka. Msaada wetu ni katika jina la BWANA, Muumba wa mbingu na dunia.