Zaburi 119:49-56
Zaburi 119:49-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Ambalo kwalo umenipa tumaini. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenipa moyo. Wenye kiburi wamenidharau mno, Lakini sikiuki sheria zako. Ninapozikumbuka hukumu zako za tangu kale, Ee BWANA, ninafarijika. Ghadhabu kuu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba yangu ya ugenini. Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee BWANA, nikaitii sheria yako. Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
Zaburi 119:49-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako, Kwa sababu umenitumainisha. Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imenihuisha. Wenye kiburi wamenidharau mno, Sikujiepusha na sheria zako. Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee BWANA, nikajifariji. Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki, Waiachao sheria yako. Amri zako zimekuwa nyimbo zangu, Katika nyumba ya ugeni wangu. Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako, Ee BWANA, nikaitii sheria yako. Hayo ndiyo niliyokuwa nayo, Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
Zaburi 119:49-56 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini. Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu. Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako. Ee BWANA, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji. Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako. Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi. Ee BWANA, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako. Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako.
Zaburi 119:49-56 Biblia Habari Njema (BHN)
Ukumbuke ahadi yako kwangu mimi mtumishi wako, ahadi ambayo imenipa matumaini. Hata niwapo taabuni napata kitulizo, maana ahadi yako yanipa uhai. Wasiomjali Mungu hunidharau daima, lakini mimi sikiuki sheria yako. Ninapoyakumbuka maagizo yako ya tangu kale, nafarijika, ee Mwenyezi-Mungu. Nashikwa na hasira kali, nionapo waovu wakivunja sheria yako. Masharti yako yamekuwa wimbo wangu, nikiwa huku ugenini. Usiku ninakukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu, na kushika sheria yako. Hii ni baraka kubwa kwangu, kwamba nazishika kanuni zako.