Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 118:1-29

Zaburi 118:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele. Watu wa Israeli na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Wazawa wa Aroni na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Wote wamchao Mwenyezi-Mungu na waseme: “Fadhili zake zadumu milele.” Katika taabu yangu nilimwomba Mwenyezi-Mungu, naye akanisikia na kuniweka huru. Mwenyezi-Mungu yuko nami, siogopi kitu; binadamu ataweza kunifanya nini? Mwenyezi-Mungu yuko nami, kunisaidia; nami nitawaona maadui zangu wameshindwa. Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kumtumainia mwanadamu. Afadhali kukimbilia usalama kwa Mwenyezi-Mungu, kuliko kuwatumainia viongozi wa dunia. Mataifa yote yalinizingira, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu nikayaangamiza! Yalinizunguka kila upande, lakini kwa jina la Mwenyezi-Mungu, nikayaangamiza! Yalinizunguka, mengi kama nyuki, lakini yakateketea kama kichaka motoni; kwa jina la Mwenyezi-Mungu niliyaangamiza! Nilishambuliwa mno karibu nishindwe, lakini Mwenyezi-Mungu alinisaidia. Mwenyezi-Mungu ni nguvu yangu kuu; yeye mwenyewe ndiye wokovu wangu. Sauti za furaha ya ushindi zasikika hemani mwao waadilifu: “Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu! Mkono wa nguvu wa Mwenyezi-Mungu umeleta ushindi! Mkono wa Mwenyezi-Mungu umetenda mambo makuu!” Sitakufa, bali nitaishi, na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ameniadhibu sana, lakini hakuniacha nife. Nifungulie milango ya watu waadilifu, niingie na kumshukuru Mwenyezi-Mungu! Huu ndio mlango wa Mwenyezi-Mungu, watu waadilifu watapitia humo. Nakushukuru, ee Mungu kwa kunijibu; kwa sababu wewe ni wokovu wangu. Jiwe walilokataa waashi, limekuwa jiwe kuu la msingi. Hiyo ni kazi yake Mwenyezi-Mungu nayo ni ya ajabu sana kwetu. Hii ndiyo siku aliyoifanya Mwenyezi-Mungu; tushangilie na kufurahi. Tafadhali utuokoe, ee Mwenyezi-Mungu! Tafadhali utufanikishe, ee Mwenyezi-Mungu! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mwenyezi-Mungu! Twawabariki kutoka nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu Mwenyezi-Mungu ni Mungu; yeye ametujalia mwanga wake Shikeni matawi ya sherehe, mkiandamana mpaka madhabahuni. Wewe ni Mungu wangu, nami ninakushukuru; ninakutukuza, ee Mungu wangu. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake zadumu milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 118

Zaburi 118:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Haleluya. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Wamchao BWANA na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Katika shida yangu nilimwita BWANA; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi. BWANA yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? BWANA yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wakiwa wameshindwa. Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia BWANA. Kuliko kuwatumainia wakuu. Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la BWANA niliwakatilia mbali. Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la BWANA niliwakatilia mbali. Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la BWANA niliwakatilia mbali. Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini BWANA akanisaidia. BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu. Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kulia wa BWANA hutenda makuu. Mkono wa kulia wa BWANA umetukuzwa; Mkono wa kulia wa BWANA hutenda makuu. Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya BWANA. BWANA ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife. Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru BWANA. Lango hili ni la BWANA, Wenye haki ndio watakaoliingia. Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu. Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa BWANA, Nalo ni ajabu machoni petu. Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA, Tutashangilia na kuifurahia. Ee BWANA, utuokoe, twakusihi; Ee BWANA, utufanikishe, twakusihi. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la BWANA; Tumewabariki toka nyumbani mwa BWANA. BWANA ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu. Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 118

Zaburi 118:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Haleluya. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Mlango wa Haruni na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Wamchao BWANA na waseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele. Katika shida yangu nalimwita BWANA; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi. BWANA yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? BWANA yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. Ni heri kumkimbilia BWANA Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia BWANA. Kuliko kuwatumainia wakuu. Mataifa yote walinizunguka; Kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Walinizunguka, naam, walinizunguka; Kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Ulinisukuma sana ili nianguke; Lakini BWANA akanisaidia. BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu, Naye amekuwa wokovu wangu. Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa BWANA hutenda makuu. Mkono wa kuume wa BWANA umetukuzwa; Mkono wa kuume wa BWANA hutenda makuu. Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya BWANA. BWANA ameniadhibu sana, Lakini hakuniacha nife. Nifungulieni malango ya haki, Nitaingia na kumshukuru BWANA. Lango hili ni la BWANA, Wenye haki ndio watakaoliingia. Nitakushukuru kwa maana umenijibu, Nawe umekuwa wokovu wangu. Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa BWANA, Nalo ni ajabu machoni petu. Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA, Tutashangilia na kuifurahia. Ee BWANA, utuokoe, twakusihi; Ee BWANA, utufanikishe, twakusihi. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la BWANA; Tumewabarikia toka nyumbani mwa BWANA. BWANA ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru. Ifungeni dhabihu kwa kamba Pembeni mwa madhabahu. Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 118

Zaburi 118:1-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. Israeli na aseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” Nyumba ya Aroni na iseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” Wote wamchao BWANA na waseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” Wakati wa maumivu yangu makuu nilimlilia BWANA, naye akanijibu kwa kuniweka huru. BWANA yuko pamoja nami, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini? BWANA yuko pamoja nami, yeye ni msaidizi wangu. Nitawatazama adui zangu wakiwa wameshindwa. Ni bora kumkimbilia BWANA kuliko kumtumainia mwanadamu. Ni bora kumkimbilia BWANA kuliko kuwatumainia wakuu. Mataifa yote yalinizunguka, lakini kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Walinizunguka pande zote, lakini kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Walinizunguka kama kundi la nyuki, lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo; kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali. Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka, lakini BWANA alinisaidia. BWANA ni nguvu yangu na wimbo wangu, yeye amefanyika wokovu wangu. Sauti za shangwe na ushindi zinavuma hemani mwa wenye haki: “Mkono wa kuume wa BWANA umetenda mambo makuu! Mkono wa kuume wa BWANA umeinuliwa juu, mkono wa kuume wa BWANA umetenda mambo makuu!” Sitakufa, bali nitaishi, nami nitatangaza yale BWANA aliyoyatenda. BWANA ameniadhibu vikali, lakini hakuniacha nife. Nifungulie malango ya haki, nami nitaingia na kumshukuru BWANA. Hili ni lango la BWANA ambalo wenye haki wanaweza kuliingia. Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu, umekuwa wokovu wangu. Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. BWANA ametenda hili, nalo ni la kushangaza machoni petu. Hii ndiyo siku BWANA aliyoifanya, tushangilie na kufurahi ndani yake. Ee BWANA, tuokoe, Ee BWANA, utujalie mafanikio. Heri yule ajaye kwa jina la BWANA. Kutoka nyumba ya BWANA tunakubariki. BWANA ndiye Mungu, naye ametuangazia nuru yake. Mkiwa na matawi mkononi, unganeni kwenye maandamano ya sikukuu hadi kwenye pembe za madhabahu. Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele.

Shirikisha
Soma Zaburi 118