Zaburi 103:9-14
Zaburi 103:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.
Zaburi 103:9-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele, yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu. Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha; kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi. Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wale wanaomcha; kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
Zaburi 103:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Hatukemeikemei daima, wala hasira yake haidumu milele. Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu. Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao. Mungu ajua mfumo wa nafsi zetu; ajua kwamba sisi ni mavumbi.
Zaburi 103:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yeye hatashutumu daima, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda kulingana na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana, kama mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Ndivyo fadhili zake zilivyo kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.