Zaburi 103:2-13
Zaburi 103:2-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako kutoka kwa kaburi, Akutia taji la fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai; BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa. Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake. BWANA amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatashutumu daima, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda kulingana na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana, kama mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Ndivyo fadhili zake zilivyo kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao.
Zaburi 103:2-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai; BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa. Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake. BWANA amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo BWANA anavyowahurumia wamchao.
Zaburi 103:2-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, wala usisahau wema wake wote, akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma, atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai. BWANA hutenda haki, naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa. Alijulisha Mose njia zake, na wana wa Israeli matendo yake. BWANA ni mwingi wa huruma na mwenye neema; si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo. Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele, yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu. Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha; kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi. Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wale wanaomcha
Zaburi 103:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote. Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake. Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao. Alimjulisha Mose mwongozo wake, aliwaonesha watu wa Israeli matendo yake. Mwenyezi-Mungu ni mwenye rehema na huruma; ni mvumilivu na mwingi wa fadhili. Hatukemeikemei daima, wala hasira yake haidumu milele. Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu. Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao.