Methali 30:24-33
Methali 30:24-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Kuna viumbe vinne vidogo sana duniani, lakini vina akili sana: Sisimizi: Wadudu wasio na nguvu, lakini hujihifadhia chakula wakati wa kiangazi; pelele: Wanyama wasio na uwezo, lakini hujitengenezea makao miambani; nzige: Hawana mfalme, lakini wote huenda pamoja kwa vikosi; mjusi: Waweza kumshika mkononi, lakini huingia katika ikulu. Kuna viumbe vitatu vyenye mwendo wa kupendeza, naam, kuna viumbe vinne vyenye mwendo mzuri; simba: Mnyama mwenye nguvu kuliko wote, wala hamwogopi mnyama mwingine yeyote; jogoo aendaye kwa maringo; tena beberu; na mfalme mbele ya watu wake. Kama umekuwa mpumbavu hata ukajisifu, au kama umekuwa unapanga maovu, chunga mdomo wako. Maana ukisukasuka maziwa utapata siagi, ukimpiga mtu pua atatoka damu; kadhalika kuchochea hasira huleta ugomvi.
Methali 30:24-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana. Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa joto. Kwanga ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba. Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi. Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme. Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri. Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hatishwi na mwingine yeyote yule; Jogoo anayetamba; na beberu; Na mfalme asimamaye mbele ya watu wake. Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako. Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.
Methali 30:24-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana. Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari. Wibari ni watu dhaifu; Lakini hujifanyia nyumba katika miamba. Nzige hawana mfalme; Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi. Mjusi hushika kwa mikono yake; Lakini yumo majumbani mwa wafalme. Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri. Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote; Jimbi aendaye tambo; na beberu; Na mfalme ambaye haasiki. Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza; Au ikiwa umewaza mabaya; Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako. Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi; Na kupiga pua hutokeza damu; kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.
Methali 30:24-33 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Vitu vinne duniani vilivyo vidogo, lakini vina akili nyingi sana: Mchwa ni viumbe wenye nguvu ndogo, hata hivyo hujiwekea akiba ya chakula chao wakati wa kiangazi. Pelele ni viumbe vyenye uwezo mdogo hata hivyo hujitengenezea nyumba zao kwenye miamba. Nzige hawana mfalme, hata hivyo huenda pamoja vikosi vikosi. Mjusi anaweza kushikwa kwa mkono, hata hivyo huonekana katika majumba ya kifalme. “Viko vitu vitatu ambavyo vinapendeza katika mwendo wao, naam, vinne ambavyo hutembea kwa mwendo wa madaha: simba, mwenye nguvu miongoni mwa wanyama, asiyerudi nyuma kwa chochote; jogoo atembeaye kwa maringo, pia beberu, naye mfalme pamoja na jeshi lake lililomzunguka. “Ikiwa umefanya upumbavu na ukajitukuza mwenyewe, au kama umepanga mabaya, basi funika mdomo wako na mkono wako. Kwa maana kama vile kusukasuka maziwa hutoa siagi, na pia kule kufinya pua hutoa damu, kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.”