Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 21:1-31

Methali 21:1-31 Biblia Habari Njema (BHN)

Moyo wa mfalme ni kama maji yanayotiririka; Mwenyezi-Mungu, huuongoza popote apendapo. Matendo yote ya mtu ni sawa machoni pake, lakini Mwenyezi-Mungu hupima mioyo. Kutenda mambo mema na ya haki, humpendeza Mwenyezi-Mungu kuliko tambiko. Macho ya kiburi na moyo wa majivuno huonesha wazi dhambi ya waovu. Mipango ya mtu wa bidii huleta mali kwa wingi, lakini kila aliye na pupa huishia patupu. Mali ipatikanayo kwa udanganyifu, ni mvuke upitao na mtego wa kifo. Ukatili wa wakatili utawafutilia mbali, maana wanakataa kutenda yaliyo ya haki. Njia ya mtu mwenye hatia imepotoka, lakini mwenendo wa mnyofu umenyooka. Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani na mwanamke mgomvi. Anachopania kutenda mtu mbaya ni uovu; hata kwa jirani yake hana huruma. Ukimwadhibu mwenye dhihaka, mjinga hupata hekima; ukimfundisha mwenye hekima, unampatia maarifa. Mungu Mwadilifu anajua wanayotenda waovu nyumbani kwao; naye atawaangusha na kuwaangamiza. Anayekataa kusikiliza kilio cha maskini, naye pia hatasikilizwa atakapolilia msaada. Hasira hutulizwa kwa zawadi ya siri; tunu apewayo mtu imefichwa hupooza ghadhabu. Haki ikitekelezwa watu wema hufurahi, lakini watu waovu hufadhaishwa. Anayetangatanga mbali na njia ya busara, atajikuta ametua miongoni mwa wafu. Anayependa anasa atakuwa maskini; anayefikiria tu kula na kunywa hatatajirika. Mwovu atapata pigo ambalo halitampata mtu mwema, mkosefu ataadhibiwa badala ya mnyofu. Afadhali kuishi jangwani, kuliko kukaa na mwanamke mgomvi na msumbufu. Nyumbani kwa mwenye busara mna hazina za thamani, lakini mpumbavu huponda mali yake yote. Anayepania uadilifu na huruma, ataishi maisha marefu na kuheshimiwa. Mwenye hekima aweza kuteka mji wa wenye nguvu, na kuziporomosha ngome wanazozitegemea. Achungaye mdomo wake na ulimi wake, hujiepusha na matatizo. Mwenye majivuno na kiburi jina lake ni “Madharau;” matendo yake yamejaa majivuno ya ufidhuli wake. Mvivu hufa kwa kutotimizwa tamaa zake, maana mikono yake milegevu haitaki kufanya kazi. Mchana kutwa mwovu hutamani kupata kitu, lakini mwadilifu hutoa, tena kwa ukarimu. Tambiko ya mwovu ni kitu cha kuchukiza, huchukiza zaidi akiitoa kwa nia mbaya. Shahidi mwongo ataangamia, lakini msikivu hawezi kunyamazishwa. Mtu mwovu hujionesha kuwa jasiri, lakini mwadilifu huhakikisha ametenda sawa. Hakuna hekima, maarifa, wala mawaidha yoyote ya mtu, yawezayo kumshinda Mwenyezi-Mungu. Farasi hutayarishwa kwa vita, lakini ushindi wamtegemea Mwenyezi-Mungu.

Shirikisha
Soma Methali 21

Methali 21:1-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA; Kama mifereji ya maji huugeuza popote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka. Mwenye kiburi na moyo wa majivuno, Taa yake ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. Matakwa yake mtu mvivu humwua, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya BWANA. Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.

Shirikisha
Soma Methali 21

Methali 21:1-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa BWANA; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu Humpendeza BWANA kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya BWANA. Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.

Shirikisha
Soma Methali 21

Methali 21:1-31 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Moyo wa mfalme uko katika mkono wa BWANA; huuongoza kama mkondo wa maji, popote apendapo. Njia zote za mwanadamu huonekana sawa kwake, bali BWANA huupima moyo. Kufanya yaliyo sawa na haki inakubalika zaidi kwa BWANA kuliko dhabihu. Macho ya kudharau na moyo wa kiburi, ambavyo ni taa ya waovu, vyote ni dhambi! Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha. Jeuri ya waovu itawaburuta mbali, kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa. Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu, bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu. Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. Mtu mwovu hutamani sana ubaya, jirani yake hapati huruma kutoka kwake. Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa, mjinga hupata hekima; wakati mtu mwenye hekima afundishwapo, hupata maarifa. Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu, naye atawaangamiza waovu. Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini, yeye pia atalia, wala hatajibiwa. Zawadi itolewayo kwa siri hutuliza hasira na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali. Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki, bali kitisho kwa watenda mabaya. Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu, hupumzika katika kundi la waliokufa. Mtu apendaye anasa atakuwa maskini, yeyote apendaye mvinyo na mafuta kamwe hatakuwa tajiri. Waovu huwa fidia kwa ajili ya wenye haki, nao wasio waaminifu kwa ajili ya wanyofu. Ni afadhali kuishi jangwani kuliko kuishi na mke mgomvi na mkorofi. Katika nyumba ya mwenye hekima kuna akiba ya vyakula vizuri na mafuta, lakini mtu mpumbavu hutafuna vyote alivyo navyo. Yeye afuatiaye haki na upendo hupata uzima, mafanikio na heshima. Mtu mwenye hekima huushambulia mji wa wenye nguvu, na kuangusha ngome wanazozitegemea. Yeye alindaye kinywa chake na ulimi wake hujilinda na maafa. Mtu mwenye kiburi na majivuno, “Mdhihaki” ndilo jina lake; hutenda mambo kwa kiburi kilichozidi. Kutamani sana kwa mvivu kutakuwa kifo chake, kwa sababu mikono yake haitaki kufanya kazi. Mchana kutwa hutamani zaidi, lakini mnyofu hutoa pasipo kuzuia. Dhabihu ya mtu mwovu ni chukizo, si zaidi sana itolewapo kwa nia mbaya! Shahidi wa uongo ataangamia, bali maneno ya mwenye kusikia yatadumu. Mtu mwovu ana uso wa ushupavu, bali mtu mnyofu huzifikiria njia zake. Hakuna hekima, wala akili, wala mpango unaoweza kufaulu dhidi ya BWANA. Farasi huandaliwa kwa ajili ya siku ya vita, bali ushindi huwa kwa BWANA.

Shirikisha
Soma Methali 21

Methali 21:1-31

Methali 21:1-31 BHNMethali 21:1-31 BHNMethali 21:1-31 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima