Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 18:1-24

Methali 18:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)

Anayetafuta yake tu hujitenga na wenzake; hukasirika akipewa shauri lolote jema. Mpumbavu hapendezwi na busara; kwake cha maana ni maoni yake tu. Ajapo mwovu huja pia dharau; pamoja na aibu huja fedheha. Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima; yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika. Si vizuri kumpendelea mtu mwovu, na kumnyima haki mtu mwadilifu. Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi; kila anachosema husababisha adhabu. Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe; mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu; ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni. Mtu mvivu kazini mwake ni ndugu yake mharibifu. Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara; mwadilifu huukimbilia akawa salama. Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake; anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda. Majivuno ya moyoni huleta maangamizi, lakini unyenyekevu huleta heshima. Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu. Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa, lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije? Mtu mwenye akili hujipatia maarifa, sikio la mwenye busara hutafuta maarifa. Zawadi humfungulia mtu milango; huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu. Ajiteteaye kwanza huonekana msema kweli, mpaka hapo mpinzani wake atakapoanza kumhoji. Kura hukomesha ubishi; huamua kati ya wakuu wanaopingana. Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome; magomvi hubana kama makufuli ya ngome. Maneno ya mtu yaweza kumshibisha; hutosheka kwa matokeo ya maneno yake. Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua; wanaopenda kuutumia watakula matunda yake. Anayempata mke amepata bahati njema; hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Maskini huomba kwa unyenyekevu, bali tajiri hujibu kwa ukali. Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu, lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu.

Shirikisha
Soma Methali 18

Methali 18:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema. Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu. Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama. Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima. Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni. Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo. Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharibifu. Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu. Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza. Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu. Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome. Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA. Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali. Ajifanyiaye marafiki wengi ni kwa maangamizi yake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.

Shirikisha
Soma Methali 18

Methali 18:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema. Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu. Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama. Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima. Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni. Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo. Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu. Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu. Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza. Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu. Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome. Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA. Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali. Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.

Shirikisha
Soma Methali 18

Methali 18:1-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Mtu ajitengaye na wengine hufuata matakwa yake mwenyewe; hupiga vita kila shauri jema. Mpumbavu hafurahii ufahamu, bali hufurahia kutangaza maoni yake mwenyewe. Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia, pamoja na aibu huja lawama. Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji, bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika. Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu, au kumnyima haki asiye na hatia. Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi na kinywa chake hualika kipigo. Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu. Mtu aliye mlegevu katika kazi yake ni ndugu na yule anayeharibu. Jina la BWANA ni ngome imara, wenye haki huikimbilia na kuwa salama. Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa. Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi, bali unyenyekevu hutangulia heshima. Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza, huo ni upumbavu wake na aibu yake. Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa, masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa. Zawadi humfungulia njia mtoaji, nayo humleta mbele ya wakuu. Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi, hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali. Kupiga kura hukomesha mashindano na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana. Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika kuliko mji uliozungushiwa ngome, nayo mabishano ni kama malango ya ngome yenye makomeo. Tumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake, atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake. Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi, nao waupendao watakula matunda yake. Apataye mke apata kitu chema naye ajipatia kibali kwa BWANA. Mtu maskini huomba kuhurumiwa bali tajiri hujibu kwa ukali. Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu, bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.

Shirikisha
Soma Methali 18

Methali 18:1-24

Methali 18:1-24 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima