Wafilipi 4:8-13
Wafilipi 4:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi. Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka. Kusema kweli mmekuwa mkinikumbuka daima ila tu hamkupata nafasi ya kuonesha jambo hilo. Sisemi hivyo sasa kwa sababu nahitaji kitu; maana nimejifunza kuridhika na vitu nilivyo navyo. Najua hali ya kutokuwa na vitu na hali ya kuwa na vingi. Nimejizoeza kuridhika katika kila hali na mahali; niwe nina cha kutosha au nina njaa; iwe nina ziada au nimepungukiwa. Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu.
Wafilipi 4:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya heshima, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nilifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yoyote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yoyote, na katika mambo yoyote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
Wafilipi 4:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi. Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
Wafilipi 4:8-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Nina furaha kubwa katika Bwana Isa kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.