Wafilipi 3:1-7
Wafilipi 3:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika kuungana na Bwana. Sichoki kurudia yale niliyokwisha andika pale awali, maana yatawaongezeeni usalama. Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa, watu wanaosisitiza kujikata mwilini. Watu waliotahiriwa kikweli ni sisi, si wao; kwani sisi twamwabudu Mungu kwa njia ya Roho wake, na kuona fahari katika kuungana na Kristo Yesu. Mambo ya nje tu hatuyathamini. Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo: Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo, na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo.
Wafilipi 3:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana. Kuwaandikieni mambo yale yale hakuniudhi mimi, bali kutawafaa ninyi. Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao. Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili. Lakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu yeyote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nilitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, niliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
Wafilipi 3:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana. Kuwaandikieni mambo yale yale hakuniudhi mimi, bali kutawafaa ninyi. Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao. Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili. Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
Wafilipi 3:1-7 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu. Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili, ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili. Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.