Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wafilipi 1:1-30

Wafilipi 1:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Mimi Paulo na Timotheo, watumishi wa Yesu Kristo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Filipi ambao mmeunganishwa na Kristo Yesu, pamoja na viongozi na wasaidizi wa kanisa. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbukeni; na kila ninapowaombeeni nyote, nasali kwa furaha, kwa sababu ya jinsi mlivyonisaidia katika kazi ya Injili tangu siku ile ya kwanza mpaka leo. Basi, nina hakika kwamba Mungu aliyeanza kazi hii njema ndani yenu, ataiendeleza mpaka ikamilike katika siku ile ya Kristo Yesu. Hivyo ndivyo ninavyopaswa kuwafikirieni, kwani nawakumbukeni daima moyoni mwangu. Kwa maana nyinyi nyote mmeshiriki katika fadhili aliyonijalia Mungu ya kutetea na kuithibitisha Injili, sasa niwapo kifungoni na pia pale awali nilipokuwa huru. Mungu anajua kuwa ninasema ukweli ninaposisitiza kwamba, kwa upendo uleule wa Yesu Kristo, natamani sana kuwaoneni. Sala yangu ni hii: Naomba upendo wenu uzidi kuongezeka zaidi na zaidi pamoja na ujuzi wa kweli na busara ya kila namna, ili muweze kuchagua jambo lililo bora. Hapo ndipo mtakuwa safi na bila lawama yoyote ile katika siku ile ya Kristo. Maisha yenu yatajazwa mambo yote yaliyo kweli bora, ambayo Yesu Kristo mwenyewe anaweza kuwajalieni, kwa ajili ya utukufu na sifa ya Mungu. Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili. Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo. Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu. Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri. Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili. Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni. Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi, kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa. Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima. Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi; lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi. Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani. Basi, nitakapokuwa nanyi tena mtakuwa na sababu ya kuona fahari juu yangu katika kuungana na Kristo Yesu. Basi, jambo muhimu ni kwamba mwenendo wenu uambatane na matakwa ya Injili ya Kristo, ili kama nikiweza kuja kwenu au nisipoweza, nipate walau kusikia kwamba mnasimama imara mkiwa na lengo moja, na kwamba mnapigana vita kwa pamoja na mnayo nia moja kwa ajili ya imani ya Injili. Msiwaogope maadui zenu, bali muwe hodari daima, na hiyo itawathibitishia kwamba wao watashindwa, nanyi mtashinda kwani Mungu mwenyewe ndiye anayewapeni ushindi. Maana nyinyi mmepewa fadhili ya kumtumikia Kristo si tu kwa kumwamini bali pia kwa kuteswa kwa ajili yake. Sasa mwaweza kushirikiana nami katika kupigana vita. Vita hivi ni vile mlivyoona nikipigana pale awali na ambavyo bado napigana sasa kama mnavyosikia.

Shirikisha
Soma Wafilipi 1

Wafilipi 1:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo, sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha, kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata hivi leo. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu; vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; akiwa mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu. Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu. Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema. Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili; bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu. Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo; kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani; hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena. Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili; wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lolote; kwao hao ni ishara thabiti ya kuangamizwa, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu. Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba ninayo hata sasa.

Shirikisha
Soma Wafilipi 1

Wafilipi 1:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo, sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha, kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu; vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu. Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu. Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema. Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili; bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu. Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo; kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani; hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena. Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili; wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu. Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba ninayo hata sasa.

Shirikisha
Soma Wafilipi 1

Wafilipi 1:1-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Waraka wa Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu: Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu walioko Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi: Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu. Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami. Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu. Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu. Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo. Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga. Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema. Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili. Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu. Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi. Naam, nami nitaendelea kufurahi, kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui! Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi. Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili. Kwa kuwa nina matumaini haya, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani. Ili kwamba furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa kule kuja kwangu kwenu tena. Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja, wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu. Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake, kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.

Shirikisha
Soma Wafilipi 1