Hesabu 23:18-24
Hesabu 23:18-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo, Balaamu akamtolea Balaki kauli yake: “Inuka, Balaki, usikie, nisikilize ewe mwana wa Sipori. Mungu si mtu, aseme uongo, wala si binadamu, abadili nia yake! Je, ataahidi kitu na asikifanye, au kusema kitu asikitimize? Tazama, nimepewa amri ya kubariki, naye amebariki wala siwezi kuitangua. Mwenyezi-Mungu hajaona ubaya kwa wana wa Yakobo, wala udhia kwa hao wana wa Israeli. Mwenyezi-Mungu Mungu wao yuko pamoja nao, Yeye husifiwa kwa vifijo miongoni mwao, yeye huzipokea sifa zao za kifalme. Mungu aliyewachukua kutoka Misri, huwapigania kwa nguvu kama za nyati. Hakika ulozi hauwezi kuwapinga watu wa Yakobo, wala uchawi dhidi ya watu wa Israeli. Sasa kuhusu Israeli, watu watasema, ‘Tazameni maajabu aliyotenda Mungu!’ Tazama! Waisraeli wameinuka kama simba jike, wanasimama kama simba dume. Ni kama simba asiyelala mpaka amalize mawindo yake, na kunywa damu ya mawindo.”
Hesabu 23:18-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalitimiza? Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. BWANA, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme iko katikati yao. Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba jike, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hadi atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.
Hesabu 23:18-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. BWANA, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao. Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.
Hesabu 23:18-24 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake: “Balaki, inuka na usikilize, nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori. Mungu si mtu, hata aseme uongo, wala yeye si mwanadamu, hata ajute. Je, anasema, kisha asitende? Je, anaahidi, asitimize? Nimepokea agizo kubariki; amebariki, nami siwezi kubadilisha. “Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo, wala taabu katika Israeli. BWANA, Mungu wao yu pamoja nao, nayo sauti kuu ya Mfalme imo katikati yao. Mungu aliwatoa kutoka Misri; wao wana nguvu za nyati. Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo, wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli. Sasa itasemwa kuhusu Yakobo na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’ Taifa lainuka kama simba jike; linajiinua kama simba ambaye hatulii mpaka amalize kurarua mawindo yake na kunywa damu ya mawindo yake.”