Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 10:11-36

Hesabu 10:11-36 Biblia Habari Njema (BHN)

Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa, nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani. Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose. Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari. Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni. Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka. Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Reubeni, walifuata kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Shelumieli mwana wa Suri-shadai, aliliongoza kabila la Simeoni. Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliliongoza kabila la Gadi. Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohathi, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipowasili, hema lilikuwa limekwisha simikwa. Baada ya hao, walifuata watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Efraimu, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elishama mwana wa Amihudi. Gamalieli mwana wa Pedasuri aliliongoza kabila la Manase, naye Abidani mwana wa Gideoni, aliliongoza kabila la Benyamini. Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya vikosi vyote, walisafiri, kundi moja baada ya jingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai. Pagieli, mwana wa Okrani, aliliongoza kabila la Asheri. Naye Ahira mwana wa Enani, aliliongoza kabila la Naftali. Huu basi, ndio utaratibu walioufuata Waisraeli kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena. Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.” Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.” Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu. Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.” Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi. Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana. Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.” Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.”

Shirikisha
Soma Hesabu 10

Hesabu 10:11-36 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi. Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani. Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya BWANA kwa mkono wa Musa. Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya kambi ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake. Na juu ya jeshi la kabila la wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari. Na juu ya jeshi la kabila la wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele. Kisha beramu ya kambi ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai. Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao. Kisha beramu ya kambi ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi. Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. Kisha beramu ya kambi ya wana wa Dani, ambayo ilikuwa ni nyuma ya makambi yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani; Tena juu ya jeshi la kabila la wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele. Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopiga kambi, nawe utakuwa kiongozi wetu. Isitoshe, ukienda pamoja nasi, naam, mema yote ambayo BWANA atatutendea, nawe tutakutendea vivyo hivyo. Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la Agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Shirikisha
Soma Hesabu 10

Hesabu 10:11-36 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi. Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani. Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya BWANA kwa mkono wa Musa. Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake. Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari. Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele. Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao. Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani; Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele. Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho. Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote BWANA atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo. Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa BWANA safari ya siku tatu; na sanduku la agano la BWANA likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Na wingu la BWANA lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee BWANA, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. Tena hapo liliposimama, akasema, Ee BWANA, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Shirikisha
Soma Hesabu 10

Hesabu 10:11-36 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya maskani ya Ushuhuda. Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine mpaka wingu lilipotua katika Jangwa la Parani. Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la BWANA kupitia kwa Mose. Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya alama yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao. Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari, naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni. Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka. Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya alama yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao. Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni, naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi. Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilikuwa isimamishwe kabla wao hawajafika. Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya alama yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao. Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase, naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini. Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya alama yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao. Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri, naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali. Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka. Basi Mose akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Mose, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo BWANA amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja nasi tutakutendea mema, kwa maana BWANA ameahidi mambo mema kwa Israeli.” Akajibu, “Hapana, sitakwenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.” Lakini Mose akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali ambapo yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu. Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na BWANA.” Hivyo waliondoka kutoka mlima wa BWANA, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la BWANA liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. Wingu la BWANA lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini. Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Mose alisema, “Ee BWANA, inuka! Watesi wako na watawanyike; adui zako na wakimbie mbele zako.” Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema, “Ee BWANA, rudi, kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”

Shirikisha
Soma Hesabu 10