Nehemia 9:1-5
Nehemia 9:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wa saba, watu wa Israeli walikusanyika, wakifunga na kuvaa mavazi ya magunia na kujipaka udongo kichwani kuonesha majuto yao. Wakati huo, walikuwa wamejitenga mbali na watu wa mataifa mengine, wakasimama na kuungama dhambi zao na maovu ya babu zao. Kwa muda wa kama masaa matatu, walisimama huku sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, inasomwa. Na kwa masaa matatu yaliyofuata, walikuwa wakitubu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Kuliwekwa jukwaa la Walawi; hapo walisimama Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Wakamwomba kwa sauti kubwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao. Walawi, yaani: Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabuea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakawaambia watu; “Simameni na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msifuni milele na milele! Na watu walisifu jina lako tukufu, ambalo hutukuka kuliko baraka na sifa zote.”
Nehemia 9:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani. Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao. Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha Torati ya BWANA, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama na kumwabudu BWANA, Mungu wao. Ndipo wakasimama katika jukwaa la Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia BWANA, Mungu wao, kwa sauti kuu. Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi BWANA, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.
Nehemia 9:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani. Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao. Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha torati ya BWANA, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama, wakamwabudu BWANA, Mungu wao. Ndipo wakasimama madarajani pa Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia BWANA, Mungu wao, kwa sauti kuu. Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi BWANA, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.
Nehemia 9:1-5 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi ule ule, Waisraeli walikusanyika pamoja, wakifunga na kuvaa nguo za gunia na kujitia mavumbi vichwani mwao. Wale wa uzao wa Israeli walijitenga na wageni wote. Wakasimama mahali pao, na kuungama dhambi zao na uovu wa baba zao. Wakasimama pale walipokuwa, wakasoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya BWANA Mungu wao kwa muda wa robo siku, na wakatumia robo nyingine kwa kuungama dhambi na kumwabudu BWANA Mungu wao. Walawi wafuatao walikuwa wamesimama kwenye ngazi: Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Hawa walimlilia BWANA Mungu wao kwa sauti kubwa. Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu BWANA Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele. “Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa.