Nehemia 8:1-12
Nehemia 8:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha watu wote, kwa nia moja, wakakusanyika mjini Yerusalemu kwenye uwanja ulio karibu na Lango la Maji. Wakamwambia Ezra, mwandishi, kukileta kitabu cha sheria ya Mose ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli. Ezra, ambaye alikuwa kuhani, akaenda na kukileta kitabu cha sheria ya Mose mbele ya mkutano mzima, wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuielewa hiyo sheria aliposikia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwezi wa saba. Kisha watu wote wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuelewa, Ezra aliwasomea sheria ya Mose akiwa mbele ya Lango la Maji tangu asubuhi hadi adhuhuri. Watu wote wakatega masikio yao kusikiliza kwa makini kitabu cha sheria. Ezra, mwandishi, alikuwa amesimama kwenye mimbari ya mbao iliyotengenezwa kwa kusudi hilo; na kwenye mkono wake wa kulia walikuwa wamesimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya; na kwenye mkono wake wa kushoto walikuwa wamesimama Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadana, Zekaria na Meshulamu. Ezra akasimama kwenye mimbari, mbele ya watu wote, nao wakawa wanamkazia macho yao kwa utulivu mkubwa. Mara tu Ezra alipokifungua kitabu cha sheria, watu wote wakasimama wima. Ezra akamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu na watu wote wakaitikia “Amina! Amina!” Huku wakiwa wameinua mikono yao juu. Kisha wakamsujudia Mungu huku nyuso zao zikigusa ardhi. Walawi wafuatao walisaidia kuwaelewesha watu sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya; walifanya hivyo kila mmoja akiwa amesimama mahali pake. Wakasoma vizuri toka kitabu cha sheria ya Mungu na kuifafanua na watu wote waliweza kuielewa. Watu waliposikia sheria, waliguswa mioyoni mwao, ndipo wote walipoanza kulia. Hivyo Nehemia aliyekuwa mtawala na Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliowafundisha watu waliwaambia watu wote, “Siku hii ni siku takatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hivyo msiomboleze wala kulia. Sasa rudini nyumbani mkafanye sherehe, mle vinono na kunywa divai nzuri, lakini kumbukeni kuwapelekea wale ambao hawana cha kutosha; kwani leo ni siku takatifu kwa Bwana wetu. Msihuzunike kwa sababu furaha anayowajalia Mwenyezi-Mungu itawapeni nguvu.” Hivyo, Walawi wakawatuliza watu wote, wakisema, “Tulieni kwani siku ya leo ni takatifu; msihuzunike.” Watu wote wakarudi nyumbani kwao kula na kunywa; wakifurahi na kuwagawia wengine chakula kwa kuwa waliyaelewa yote waliyotangaziwa.
Nehemia 8:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha Torati ya Musa, BWANA aliyowaamuru Israeli. Naye Ezra, kuhani, akaileta Torati mbele ya mkutano mzima, wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba. Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha Torati. Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameitengeneza kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kulia; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi BWANA, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudu BWANA kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika Torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa BWANA, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, Nendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyekuwa na kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya BWANA ni nguvu zenu. Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.
Nehemia 8:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, BWANA aliyowaamuru Israeli. Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba. Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha torati. Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu. Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi BWANA, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu BWANA kifudifudi. Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao. Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa. Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa BWANA, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati. Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya BWANA ni nguvu zenu. Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.
Nehemia 8:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Sheria ya Mose, ambacho BWANA aliamuru kwa ajili ya Israeli. Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Sheria mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu. Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko mpaka adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Sheria. Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume alisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwepo Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu. Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama. Ezra akamsifu BWANA, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu BWANA hali nyuso zao zikigusa ardhi. Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafunza ile Sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya. Walisoma kutoka kile Kitabu cha Sheria ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa. Ndipo Nehemia aliyekuwa mtawala, Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa BWANA Mungu wenu. Msiomboleze wala msilie.” Kwa kuwa watu wote walikuwa wakilia walipokuwa wakisikiliza maneno ya ile Sheria. Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa BWANA. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya BWANA ni nguvu zenu.” Walawi wakawatuliza watu wote wakisema, “Kuweni watulivu, kwa kuwa hii ni siku takatifu. Msihuzunike.” Kisha watu wote wakaondoka kwenda kula na kunywa, na kupeana sehemu ya chakula, na wakaadhimisha kwa furaha kubwa, kwa sababu sasa walifahamu maneno yale waliyokuwa wameelezwa.