Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 9:17-27

Marko 9:17-27 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

Mtu mmoja miongoni mwa umati ule wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea. Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.” Isa akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini! Nitakuwa pamoja nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana kwangu.” Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Isa, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani. Isa akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake. Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.” Isa akamwambia, “Ati, ‘Kama unaweza kufanya jambo lolote’? Yote yawezekana kwake yeye aaminiye.” Mara baba yake yule mvulana akapaza sauti akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!” Isa alipoona kwamba umati wa watu wanakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!” Baada ya yule pepo mchafu kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.” Lakini Isa akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.

Shirikisha
Soma Marko 9