Marko 9:1-13
Marko 9:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.” Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.” Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka kwa wafu. Wakamwuliza Yesu, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” Naye akawajibu, “Naam, Elia anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake.”
Marko 9:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu. Baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimetameta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejesha upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa sana na kudharauliwa? Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.
Marko 9:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu. Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejeza upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.
Marko 9:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.” Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao. Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu yeyote duniani angaliweza kuyangʼarisha. Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Rabi, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana. Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.” Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Yesu. Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoona, mpaka Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?” Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?” Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa? Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”