Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 8:27-38

Marko 8:27-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.” Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.” Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake. Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba atauawa, na baada ya siku tatu atafufuka. Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Hapo, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, “Ondoka mbele yangu Shetani! Mawazo yako si ya kimungu ila ni ya kibinadamu.” Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu anayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa. Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake? Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake? Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisicho na uaminifu kwa Mungu, anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo, wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Shirikisha
Soma Marko 8

Marko 8:27-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yesu na wanafunzi wake wakaondoka kwenda katika vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?” Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema wewe ni mmojawapo wa manabii.” Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo.” Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake. Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuke. Aliyasema haya waziwazi, ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea. Lakini Yesu alipogeuka na kuwaangalia wanafunzi wake, akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Ndipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Shirikisha
Soma Marko 8

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha