Marko 7:14-23
Marko 7:14-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe. Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.” Mwenye masikio na asikie! Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi, kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.) Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi. Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”
Marko 7:14-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [ Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Marko 7:14-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [ Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Marko 7:14-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili. Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]” Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”) Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”