Marko 7:1-37
Marko 7:1-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake, wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasiponawa, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu chochote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokezana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [ Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake ana pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Mgiriki, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, nenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka. Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka ziwa la Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.
Marko 7:1-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake, wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba. Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo. Akawaita makutano tena, akawaambia, Nisikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. [ Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi. Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka. Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi, akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.
Marko 7:1-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Yesu. Wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani, bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi. (Kwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao. Wanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi nyingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.) Kwa hiyo wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?” Yesu akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa: “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Huniabudu bure, nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’ Ninyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.” Naye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu! Kwa mfano, Mose alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu), basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake. Kwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.” Yesu akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili. Hakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ Kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]” Akiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? Mtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Yesu alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”) Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.” Ndipo Yesu akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. Mara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria. Akamsihi Yesu amtoe binti yake huyo pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.” Ndipo Yesu akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.” Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka. Kisha Yesu akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. Huko, watu wakamletea Yesu mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye. Baadaye Yesu akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Yesu akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. Ndipo Yesu akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” (yaani, “Funguka!”) Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. Walistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”
Marko 7:1-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadhi ya Mafarisayo na waalimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: Hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. Tena, hawali kitu chochote kutoka sokoni, mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizozipokea toka zamani kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba. Basi, Mafarisayo na waalimu wa sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati mapokeo tuliyoyapokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?” Yesu akawajibu, “Wanafiki nyinyi! Nabii Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu alipoandika: ‘Mungu asema: Watu hawa, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao, wako mbali nami. Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’ Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.” Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu! Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’. Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu), basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’. Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.” Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe. Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.” Mwenye masikio na asikie! Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi, kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.) Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi. Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.” Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.” Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!” Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka. Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.” Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: Amewajalia viziwi kusikia, na mabubu kusema!”