Marko 6:14-56
Marko 6:14-56 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, “Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu, ndiyo maana nguvu hizi zinafanya kazi ndani yake.” Wengine walisema, “Mtu huyu ni Elia.” Wengine walisema, “Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale.” Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.” Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake. Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.” Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze. Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana. Ndipo ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya. Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, “Niombe chochote utakacho, nami nitakupa.” Tena akamwapia, “Chochote utakachoniomba, nitakupa; hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.” Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, “Niombe nini?” Naye akamjibu, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, “Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia. Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani, akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini. Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha. Yesu akawaambia, “Twendeni peke yetu mpaka mahali pa faragha mkapumzike kidogo.” Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno waliokuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha. Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika. Aliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi. Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa. Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Nao wakamwuliza, “Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari 200, na kuwapa chakula?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni kutazama.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi. Nao wakaketi makundimakundi ya watu 100 na ya watu hamsini. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote. Watu wote wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume 5,000. Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ngambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu. Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali. Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu. Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji, akataka kuwapita. Lakini walipomwona akitembea juu ya maji, walidhani ni mzimu, wakapiga yowe. Maana wote walipomwona waliogopa sana. Mara Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Kisha akapanda mashuani walimokuwa, na upepo ukatulia. Nao wakashangaa sana, kwa sababu hawakuwa bado wameelewa maana ya ile mikate. Akili zao zilikuwa bado zimepumbazika. Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Walipotoka mashuani watu walimtambua Yesu mara. Basi, kwa haraka wakazunguka katika nchi ile yote, wakaanza kuwachukua wagonjwa wamelala juu ya mikeka yao, wakawapeleka kila mahali waliposikia Yesu yupo. Kila mahali Yesu alipokwenda, vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa uwanjani, wakamsihi waguse walau pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.
Marko 6:14-56 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa limeenea, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo, ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asiweze. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lolote utakalo, nitakupa. Akamwapia, lolote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini. Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njooni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili. Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandalie; na wale samaki wawili akawagawia wote. Wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. Na walioila ile mikate walikuwa wanaume elfu tano. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng'ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa unwakabili; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni mzuka, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle katika mashua walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito. Hata walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani waliokuwa wagonjwa, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse angaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.
Marko 6:14-56 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini. Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili. Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote. Wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaida, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yu peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito. Hata walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapon
Marko 6:14-56 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.” Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.” Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!” Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza, kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta. Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani. Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.” Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?” Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.” Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani, akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohana walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini. Wale mitume wakakusanyika kwa Yesu na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. Basi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.” Hivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi. Mchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana. Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.” Lakini Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.” Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200 ili tuwape watu hawa wale?” Akawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.” Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Kisha Yesu akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. Watu wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000. Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. Baada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba. Ilipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. Akawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, lakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, kwa sababu wote walipomwona waliogopa. Mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!” Akapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, kwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu. Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Yesu. Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Yesu yupo. Kila mahali Yesu alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.