Marko 6:14-29
Marko 6:14-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, “Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu, ndiyo maana nguvu hizi zinafanya kazi ndani yake.” Wengine walisema, “Mtu huyu ni Elia.” Wengine walisema, “Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale.” Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.” Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake. Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.” Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze. Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana. Ndipo ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya. Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, “Niombe chochote utakacho, nami nitakupa.” Tena akamwapia, “Chochote utakachoniomba, nitakupa; hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.” Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, “Niombe nini?” Naye akamjibu, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, “Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia. Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani, akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Marko 6:14-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa limeenea, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo, ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asiweze. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lolote utakalo, nitakupa. Akamwapia, lolote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Marko 6:14-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Mfalme Herode akasikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohana Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohana, niliyemkata kichwa, amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Marko 6:14-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Yesu lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yohana Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.” Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.” Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yohana Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!” Kwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yohana Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. Yohana alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yohana kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza, kwa sababu Herode alimwogopa Yohana akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta. Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani. Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.” Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.” Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?” Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.” Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yohana. Akaenda na kumkata Yohana kichwa humo gerezani, akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. Wanafunzi wa Yohana walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.